Mshumaa wa Bwana
Revival Keys > Juma la 3 > Dokezo
 |
|
Dokezo:
Karibu tena. Juma hili, tunaangalia sharti lingine muhimu la uamsho. Na hii ni mada muhimu ilioje: kudumu kuomba. Ingawa hakuna chochote tunachohitaji kuliko kumiminiwa kipimo kikubwa zaidi cha Roho Mtakatifu, mara nyingi ndilo jambo tunaloliombea kidogo sana. Jinsi gani ambavyo malaika wa mbinguni lazima washangae wakati mwingine!
Kwa kweli, kuna sababu. Maombi halisi ni kumfungulia Mungu mioyo yetu. Kumruhusu aingie na kutuonesha hali yetu halisi, hitaji letu la kweli. Na hiyo inaweza kuwa suala lenye uchungu sana kufanya. Mwelekeo wetu wa kibinadamu ni kuepuka kwa gharama zozote aina hii ya kukutana na Mungu.
Lakini uamsho katika kiini chake ni kukutana na Mungu. Daima huangaza nuru ndani ya mianya ya giza kwenye tabia yetu. Ambapo humaanisha, uamsho huwajia tu wale walio tayari kukabiliana na Mungu katika maombi...
Mhariri,
Amefichwa katika Kristo |
These resources are licensed for personal study by . Please do not distribute.
Copyright © 2026, FAST Missions, All rights reserved. WWW.FAST.ST
Mshumaa wa Bwana
Revival Keys > Juma la 3 > Malengo
| Jina: |
|
|
Imesainiwa na: |
| Tarehe: |
|
 |
Uchunguzi wetu wa Biblia juma hili unatazama I Wafalme 18:36-39. Ni ibara fupi ya maandiko—kimsingi ni sala moja. Lakini ilisababisha moja ya matukio ya uamsho wenye nguvu zaidi katika Agano la Kale. Zaidi ya hayo, nadhani utagundua kwamba una mantiki ya wakati wa mwisho pia. Ingia, na ufurahie! |
 |
Mapendekezo Sadifu ya juma hili yana kichwa cha habari kisemacho Katika Kujibu Maombi. Soma habari hii nzima kwa maombi, ukimsihi Mungu akusaidie kutathmini maisha yako ya maombi kwa usahihi. Weka azma ya kufanya mabadiliko yoyote ambayo Mungu anakugusia moyoni mwako. |
 |
Aya yako ya kukariri juma hili pengine haifahamiki sana kuliko baadhi ya mengine tuliyoyateua, lakini hufungamana vyema na kichwa cha habari cha somo hili: Mithali 20:27. Tumia aya hii kama motisha ya kuuchunguza moyo wako kadiri tunapoendelea na harakati zetu za uamsho. |
 |
Nyenzo ya ziada za juma hili hubainisha Funguo za Maombi ya Pamoja. Zisome kwa umakini, halafu njoo kwenye mkutano wako unaofuata wa timu ukiwa umejiandaa kuzijaribu. Ikiwa hujawahi kamwe kufanya hivi hapo awali, kuwa na hakika kwamba unaelekea kupata kitu chenye manufaa makubwa. |
 |
Kwa kuwa lengo letu juma hili liko kwenye maombi, hebu tuongeze mambo kidogo. Ikiwa bado haujafanya hivyo, ongeza hitaji la maombi kwenye shajara yako ya maombi, mahususi kwa ajili ya uamsho. Hata bora zaidi, lisogeze mbele kabisa kwenye furushi lako. Kisha weka azma ya kuliombea kila siku! |
FAST
Kuomba Hazina za Kiroho kwa Bidii
Mshumaa wa Bwana
Revival Keys > Juma la 3 > Kuchunguza Maandiko
Mada: I Wafalme 18:36-39
Muhtasari Mfupi:
Maoni/Dondoo:
Kanuni & Matumizi:
Wazo Kuu:
Mshumaa wa Bwana
Revival Keys > Juma la 3 > Mapendekezo ya Kivitendo
Katika Kujibu Maombi
Uamsho huja tu katika kujibu maombi. Hiyo ni kwa sababu maombi pekee yanaweza kututayarisha kwa ajili ya uamsho. Kuichunguza Biblia kunaweza kutuonesha hali yetu halisi, lakini ni kupitia sala tu ndipo tunaweza kuuleta moyo wetu kwa Yule anayeweza kutuponya. Kwa hivyo ikiwa una nia ya dhati juu ya uamsho, lazima ujitahidi kuingia kwa undani zaidi katika shani za maombi.
Kwa kweli, kukua katika maombi siyo rahisi. Wengi hutamani maisha ya maombi ya kina zaidi, lakini hawana hakika hasa jinsi gani walifanikishe hilo. Ibara zilizo mbeleni zinaweza kusaidia, kwa kukupa dondoo muhimu za jinsi unavyoweza kujaza muda wako wa maombi kwa uwepo zaidi wa Roho. Fuata vidokezo hivi kwa uangalifu, navyo vitafanya maombi yawe sehemu ya dhati na yenye bidii zaidi maishani mwako.
Kupangilia Mambo
Kupangilia maombi yako katika shajara ya maombi ni hatua kuu ya kwanza katika kuimarisha maisha yako ya maombi. Tunapendekeza kutumia daftari lenye kurasa zisizoshikamana na kuhifadhi kila ombi kwenye karatasi tofauti. Kila karatasi kinapaswa kujumuisha ombi, aya mmoja au mbili mahususi, na kumbukumbu ya tarehe unapoiombea, pamoja na maelezo ya kina kuhusu jinsi Mungu anavyofanya kazi. Tunapendekeza utenganishe hitaji lako liwe katika sehemu moja kwa ajili ya mahitaji ya kila siku, ya kipaumbele, na nyingine kwa ajili ya mahitaji ya kawaida unayoyaombea mara chache. Ikiwa umefanya kozi yetu ya
Mafunzo Msingi, unajua shajara ya maombi inaweza kuwa na ufanisi katika kukukumbusha kuombea mambo ambayo vinginevyo ungesahau.
Lakini shajara ya maombi inaweza kuimarisha maisha yako ya maombi kwa njia zingine, ukiitumia kwa usahihi. Haya hapa mambo matatu ya kutathmini katika matumizi yako ya shajara ya maombi:
- Je, kuna mchanganyiko mzuri wa mahitaji katika shajara yako ya maombi? Ikiwa unaombea mahitaji binafsi tu, na marafiki au jamaa wachache wanaopitia changamoto, pengine ukawa unafikiria mawazo duni sana. Weka hitaji la kukua katika ubora fulani wa kitabia. Au kwa ajili ya ushindi mkubwa zaidi dhidi ya jaribu fulani linalokutesa. Ombea malengo muhimu, miradi kazini, au maongozi kwenye maamuzi fulani makubwa. Ombea uinjilisti katika nchi fulani maalum, au kwa ajili ya huduma fulani unayoiheshimu. Ongeza majina ya watu mahususi ambao ungependa kuona wakija kwa Kristo. Au ambao wanahangaika kiroho. Na kwa kweli, weka hitaji kwa ajili ya uamsho. Kadiri unavyounganisha maombi kwenye kila sehemu ya maisha yako ndivyo yatakavyokuwa na maana zaidi.
- Angalia madokezo yako. Je, unaandika tarehe tu kila wakati unapoomba? Au unaandika dondoo pia zinazohusiana na kila hitaji unapoomba? Maombi yanahusu hasa kusikia kama vile yanavyohusu kuzungumza. Kwa hiyo jaribu kujifunza kusikiliza sauti ya Mungu unapoomba. Je, Mungu anafanya kazi kwa namna fulani? Andika hilo. Je, kuna hatua fulani Mungu angependa uichukue? Iandike. Je, Mungu amekupa utambuzi fulani kuhusu sababu za hali hiyo? Au mapenzi Yake yanaweza kuwa nini? Andika hilo. Maombi huwa na nguvu zaidi yanapobadilika kuwa mawasiliano ya njia mbili. Na mara nyingi, ni yale mawasiliano yanayoleta majibu.
- Durusu aya zilizotumika katika mahitaji yako ya maombi. Je, hitaji lako liliibuliwa na aya fulani uliyoipata kwa nasibu kwenye harakati yako binafsi ya kuichunguza Biblia? Au ulipata hitaji fulani, kisha ukatafuta aya inayoonekana kulandana? Au kwa kuiweka tofauti, hivi unamwambia Mungu nini cha kufanya? Au Mungu anakuambia uombee nini? Kujifunza kumtafuta Mungu ili atuoneshe makusudi Yake, na kisha kujaribu kuelekeza mahitaji yetu kwenye makusudi hayo, kunaweza kuleta mapinduzi katika maisha yetu ya maombi na kuyageuza kuwa safari ya kusisimua. Kwa ufupi, jaribu kujumuisha mahitaji zaidi yaliyovuviwa na Maandiko.
Ingawa shajara ya maombi ni nyenzo madhubuti, manufaa yake halisi huja kwa kukufundisha jinsi ya kuunganisha maombi na kila sehemu ya maisha yako, jinsi ya kumtambua Mungu akitenda kazi katika kujibu maombi yako, na jinsi ya kuunganisha maombi yako kwa karibu zaidi na Maandiko. Aina hii ya maombi ni ufunguo wa uamsho.
Kuomba kwa Kufuatisha Maandiko
Tunapokua katika mwenendo wetu wa kutembea na Mungu, muunganiko kati ya Maandiko na maombi huwa na mwelekeo wa kuwa dhahiri zaidi na zaidi. Tunaona jinsi ambavyo kuichunguza Biblia kwa kina kunahitaji mtazamo wa kina wa maombi. Na vilevile, tunatambua namna ambavyo Mungu anazungumza nasi kupitia Maandiko, tunapowasilisha mahitaji yetu. Hatimaye, muunganiko kati ya maombi na Maandiko huwa wa kina, huwa vigumu kuvitofautisha.
Ambapo hupendekeza thamani ya kutumia Maandiko yenyewe kama mfumo wa maombi. Kivipi? Haya hapa ndiyo tunapendekeza. Kwanza, tafuta ibara ya maandiko inayoendana na hali yako kisha ifungue katika Biblia yako. Kisha, pitia tu ibara hiyo aya kwa aya, ukitumia dakika moja au mbili kuzungumza na Mungu kuhusu kile ambacho kila aya husema, ukiibinafsisha, na kuinasibisha kwenye hitaji lako mahususi. Na kisha msikilize Mungu ajibu kupitia aya hiyo. Baada ya muda mfupi, endelea kwenye aya inayofuata. Nenda haraka au polepole kadiri upendavyo.
Ikiwa unataka kujikita katika kujenga tabia, nenda kwenye fanakaheri na umwombe Mungu ajenge kila moja ya sifa hizo maishani mwako. Au unaweza kuomba kupitia Amri Kumi, na kumsihi Mungu auchunguze moyo wako ili afichue mifuko ya dhambi ambayo huenda huijui. Au unaweza kuomba kupitia Waefeso 6, na kumsihi Mungu akuimarishe kwa kukupatia kila silaha ya kiroho iliyoorodheshwa hapo. Na huo ni mwanzo tu.
Zaburi nyingi zinafaa sana kwa ajili ya vipindi vya kusifu. Zingine kwa ajili ya nyakati za kukiri, na zingine kwa ajili ya nyakati za zahama. Jaribu kuomba kupitia makundi ya mithali—ukimwomba Mungu hekima ya kiungu. Nyaraka za Paulo zimejaa maombi ya kustaajabisha ili mapenzi ya Mungu yatimizwe maishani mwa wale aliokuwa akiwandikia. Omba haya kwa ajili yako mwenyewe, au uyatumie kumwombea rafiki fulani. Na kuna maombi mengi ambayo waandishi wa Biblia waliyorekodi katika Maandiko na ambayo yanaweza kutumika kama vielelezo vya mahitaji mengine. Hata mifano na visa vya Biblia vinavyojulikana, wakati mwingine vinaweza kunasibishwa ili viendane na hali mbalimbali maishani mwako. Kadiri unapotazama zaidi, ndivyo utapata zaidi.
Kutenga nyakati maalum kwa ajili ya aina hii ya maombi kutapeleka maombi yako katika kiwango kipya kabisa. Hubadilisha maombi kuwa nyakati za kukutana na Mungu ndani ya Neno.
Maombi ya Uamsho
Shajara ya maombi ni njia bora ya kupangilia maombi yako, na inaweza kukufundisha masomo muhimu kuhusu maombi. Kuomba Kimaandiko ni njia yenye nguvu ya kumtafuta Mungu kwenye mada mahususi ukitumia Biblia yenyewe. Lakini namna kuu kabisa ya maombi inaweza kuwa maombi ya uamsho wenyewe.
Ikiwa tunakusudia kwa dhati kuutafuta uamsho, huanza na mioyo yetu wenyewe. Kumsihi Mungu atukirimie uwezo wa Roho Mtakatifu, hututaka tuwe wawazi mbele ya Mungu. Kumruhusu aangaze nuru kwenye pembe za ndani kabisa za mioyo yetu. Ili kutuonesha mawazo na dhamira zetu zilizofichika. Nia zinazotusukuma. Ikiwa unataka kumiminiwa Roho wa Mungu, lazima ujifunze kuawana na Mungu. Na hilo huchukua muda.
Fanya hatua hii ya kuawana iwe kipaumbele kila siku. Mwombe Mungu akupe ule moyo uliojisalimisha kikamilifu. Na usiache kuomba hadi uamsho uje...
Kumbuka: Kwa taarifa zaidi kuhusu mbinu mbalimbali za maombi, na kuchunguza baadhi ya maombi makuu katika Biblia, angalia miongozo yetu ya kujifunza iitwayo Nguvu katika Maombi, kwa kututembelea katika WWW.FAST.ST.
Mshumaa wa Bwana
Revival Keys > Juma la 3 > Nyenzo za Ziada
Funguo za Maombi ya Pamoja
Kuomba peke yako ni muhimu, lakini kuomba pamoja na wengine huleta baraka zake. Yesu alibainisha ahadi ambazo hasa zinahusiana na maombi ya pamoja (Mathayo 18:19-20), na kitabu cha Matendo kinaonesha wazi nguvu zake (Matendo 1:14, 2:1, 4:31). Moja ya njia bora zaidi katika kuhimiza maombi thabiti ya pamoja ni kusali kimazungumzo. (Wakati mwingine hii inaitwa maombi ya bisi, au maombi ya sentensi). Haya hapa maelezo mafupi ya jinsi yanavyofanya kazi:
- Teua kiongozi wa kuanza na kumaliza sala. Mtu huyu pia anaweza kubadilisha kikundi kupitia kila sehemu ya sala.
- Fuata mwendelezo wenye mpangilio. Tunashauri uanze kwa wasaa wa ibada, nenda kwenye hatua ya kukiri hitaji letu, kisha maombezi, na mwisho shukrani. Kiongozi hutangaza kila hatua ya mpito.
- Kila mtu huomba kadiri anavyoongozwa na Roho Mtakatifu. Wala hahitaji kuomba kwa mpangilio wowote, na anaweza kuomba mara nyingi kadiri apendavyo.
- Ifanye kila sala iwe fupi—sentensi moja au mbili tu kwa wakati. Ombea jambo moja, kisha wapatie wengine nafasi ya kuomba. Wengine wanaweza kutaka kuthibitisha ombi la mtu mwingine. Epuka maombi marefu binafsi.
- Usitumie virai rasmi ili kuanza na kuhitimisha kila sala binafsi—kama vile "Baba uliye mbinguni" au "Katika jina la Yesu." Yote ni sala moja, inayoombwa pamoja kama kikundi.
- Kuwa huru kunukuu aya ya Maandiko au mstari katika wimbo unaofahamika ikiwa Roho Mtakatifu atakugusa kufanya hivyo.
- Usikereke kwa vipindi vya ukimya. Kadiri maombi ya aina hii yanavyokuwa ya asili zaidi, wanakikundi waoga wataanza kujiunga na ukimya utapungua. Badala yake, tumia ukimya huo kumuuliza Mungu kile ambacho angetaka WEWE ukiombee.
- Wakati wa kuhitimisha unapowadia, mtu aliyeteuliwa awasilishe maombi yote kwa Mungu katika jina la Yesu—hivyo kuweka wazi kwamba kipindi cha maombi kimefika mwisho.
Jaribu mbinu hii, na punde utagundua kwamba kufanya maombi kama haya katika kikundi huweza kufungamanisha mioyo yenu pamoja kwa namna zenye nguvu.