Vielelezo

Kozi Mafunzo ya Msingi > Juma la Vielelezo > Dokezo

     

Dokezo:


Vielelezo vinavyopatikana katika kijitabu hiki ni sehemu muhimu ya Mafunzo ya Msingi—kwa kuwa vinanasa kanuni muhimu zaidi za programu husika, kwa njia ambayo ni rahisi kukumbuka na nyepesi kuiwasilisha kwa wengine. Pia vina vidokezo vya kina kuhusu maisha bora ya Kikristo. Kadiri unavyoziweka kwa uangalifu akilini mwako, na kufikiria maana zake, ndivyo matokeo yake yatakuwa makubwa zaidi maishani mwako.

Kwa kawaida vielelezo hivi huwasilishwa na kiongozi wa timu (bila maelezo) wakati wa mikutano ya mara kwa mara ya timu na kunakiliwa na wanakikundi kwenye ukurasa wa mwisho wa vijitabu vyao vya mafunzo. Kisha kijitabu hiki hutolewa baada ya kielelezo cha mwisho kuwasilishwa (juma la saba) ili kuwasaidia wanatimu katika mapitio yao kwa ajili ya kipindi cha mwisho.

Unapojifunza vielelezo hivi, mwombe Mungu akupe nafasi ya kuwashirikisha wengine wasio kwenye timu yako. Kwa kufanya hivyo, unaweza tu kufanikiwa kumvutia rafiki fulani akafanya kozi nzima ya Mafunzo ya Msingi. Hebu Mungu akujalie baraka tele unapotafuta kumfanyia kazi!

Mhariri,
Amefichwa katika Kristo

These resources are licensed for personal study by . Please do not distribute.
Copyright © 2026, FAST Missions, All rights reserved. WWW.FAST.ST

Vielelezo

Kozi Mafunzo ya Msingi > Juma la 1


Gurudumu la Mwanafunzi




Gurudumu la Mwanafunzi ni kielelezo cha thamani, kinachobainisha funguo za maisha ya kila siku yaliyojaa Roho. Ni muhimu hasa katika kuwasaidia waumini kudumu kwenye njia ya uanafunzi binafsi.

Rimu ya Nje: Hii huwakilisha maisha yetu ya kila siku: maneno, matendo, na mitazamo ambayo wengine huona ndani yetu. Ni kupitia maisha haya ya nje ndipo Kristo anaakisiwa kwa wengine.

Habu: Nguvu za maisha ya kila siku yaliyojaa Roho hutokea ndani—Kristo akaaye moyoni. Kristo ndiye hututia moyo, na kutuwezesha kuishi kwa ajili Yake.

Spoku: Ili kuipitisha nguvu hiyo kutoka kwenye habu hadi kwenye rimu, spoku nne muhimu lazima ziundiwe kwenye maisha. Hizi ni pamoja na maombi, Neno, utii, na kushuhudia. Tutakuwa tukijifunza kuhusu spoku hizi nne katika Mafunzo ya Msingi ya FAST.

Vielelezo

Kozi Mafunzo ya Msingi > Jum la 2


Baiskeli ya Kesha la Asubuhi




Baiskeli ya Kesha la Asubuhi hubainisha muhtasari wa funguo mbili za mafunzo ya Biblia ambazo ni muhimu na zenye manufaa.

Gurudumu la Mbele: Kutafakari. Mungu anatamani kuyapatia maisha yetu mwelekeo kupitia kutafakari Maandiko. Kutafakari ni kufikiria kwa kina maneno ya Biblia katika jitihada ya kugundua kanuni za kibiblia: maagizo ya maadili yanayoongeza vipengele vya kila siku vya maisha yetu. Zaburi 119:33-34.

Gurudumu la Nyuma: Matumizi. Badiliko huja tu maishani mwetu, hata hivyo, tunaposonga mbele katika kutumia Maandiko kwa njia za vitendo. Jambo muhimu ni kubadilisha kanuni kuwa miradi mahususi, midogo-midogo ambayo inaweza kufanywa na mtu binafsi. Kulitumia Neno maishani kunahitaji sisi kujibu maswali: nani, nini, lini, wapi, na jinsi gani. Zaburi 119:59-60

Vielelezo

Kozi Mafunzo ya Msingi > Juma la 3





Upinde wa Ahadi


Upinde wa Ahadi ni kielelezo chenye manufaa kinachobainisha muhtasari wa vipengele muhimu katika maombi, pamoja na nguvu zake kuu.


Upinde: Kila ahadi ya Maandiko, ni kama upinde wenye nguvu unaoweza kutumika (mara kwa mara) “kurushia” maombi yetu kwenda kwa Mungu. Ni ahadi zinazotupa uwezo wa kufikisha maombi yetu katika umbali mkubwa.

Mshale: Maombi yanapaswa kuchongoka vyema kama mshale—sahihi na mahususi. Na lazima zishikiliwe karibu na upinde—Neno la Mungu. Yaani, maombi yetu yanapaswa kushikamanishwa vilivyo kwenye Maandiko.

Kamba: Kudhihirisha imani yetu ni kama kuvuta kamba kwenye upinde. Kadiri tunapowasilisha mahitaji yetu kwa Bwana, tukitumia muda wa kupatanisha mioyo, akili, na utashi wetu kwenye Neno, Mungu anaweza kutenda kazi. Kadiri tunavyovuta kamba kwa bidii zaidi, ndivyo mshale wetu utakavyoruka kwenda mbali zaidi.

Vielelezo

Kozi Mafunzo ya Msingi > Juma la 4


Uma




Kielelezo cha Uma kinaangazia funguo za usimamizi wa muda. Hupendekeza funguo nne za kushughulikia mrundikano wa majukumu maishani mwako.

Miradi: Kwanza, azimu kutumia dakika chache kila siku, ukimkabidhi Mungu kazi unazohisi unahitaji kufanya siku hiyo. Angependa ufanye miradi gani?

Kupanga: Kisha, azimu kutumia dakika chache za ziada kila juma, ukipanga kwa maombi mambo ya juma linalofuata. Weka malengo ya juma husika. Sahisisha kipangalio chako. Angalia matukio yajayo kwenye kalenda yako.

Vipaumbele: Kisha, tenga muda kidogo kila mwezi kuchanganua vipaumbele vyako halisi. Hivi unawekeza maisha yako katika mambo ambayo ni muhimu hasa? Maadili yako yanapatana na Maandiko?

Kusudi: Hatimaye, tenga muda fulani wa kutosha angalau mara moja kila mwaka, kuombea utume wako maishani. Andika muhtasari wa uelewa wako wa kusudi la Mungu juu ya uwepo kwako—kwa sentensi moja.

Kujifunza kuweka ahadi hizi kila siku, juma, mwezi na mwaka, kutakusaidia kuweka udhibiti wa muda wako.

Vielelezo

Kozi Mafunzo ya Msingi > Juma la 5


Kanuni ya Kukariri Maandiko





Kanuni ya Kukariri Maandiko huangazia baadhi ya funguo muhimu zaidi katika kukariri Maandiko kwa ufanisi. Fuata kanuni hizi rahisi ili kudumisha uimara wa programu yako ya kukariri Maandiko:

KM=Kukariri Maandiko

M1=Mtazamo
     Azimu kukariri, bila kujali ugumu.
     Mtumaini Mungu aliandike Neno Lake moyoni mwako kwa ufanisi.

M2=Mazoezi ya Kukariri
     Jifunze kukariri kwa mwendelezo thabiti, ukitumia kifurushi cha
     aya.
     Daima kariri aya kwa usahihi.

M3=Mazoea ya Kutafakari
     Gundua maarifa katika kila aya unayojifunza.
     Yatumie maishani mwako kwa njia mahususi, za kivitendo.

R=Rudia Kila Siku
     Fanya marudio ya aya mpya kila siku kwa miezi miwili.
     Daima nukuu rejeleo kabla na baada.

R2=Rudia Mazoezi ya Zamani
     Fanyia kazi faili lako la marudio ya zamani kuanzia mara moja kwa
     juma hadi mara moja kwa mwezi—kutegemeana na idadi ya aya.

Vielelezo

Kozi Mafunzo ya Msingi > Juma la 6


Dondoo za Biblia




Dondoo za Biblia ni kielelezo rahisi unachoweza kutumia ili kuiwasilisha Injili haraka na kwa uwazi inapohitajika. Inajumuisha kweli tatu muhimu:

A. Lazima kila mmoja wetu AKIRI kwamba tumetenda dhambi na kupungukiwa mapenzi kamili ya Mungu kwa ajili ya maisha yetu. Warumi 3:23. (Angalia pia Isaya 59:2, Yeremia 13:23).

B. Lazima kila mmoja wetu AAMINI kwamba Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, na kwamba kifo Chake kilimaliza adhabu tunayostahili. Warumi 5:8. (Angalia pia I Petro 3:18, Isaya 53:6).

C. Lazima kila mmoja wetu ADAI uwezo wa Roho Mtakatifu kuongoza, kuimarisha, na kubadilisha maisha yetu ya kila siku. Warumi 8:14. (Angalia pia Ezekieli 36:27, Wagalatia 5:22-23).

Kumbuka: Hii pia wakati mwingine inaitwa Barabara ya Warumi, kwa sababu inakupitisha kwenye aya tatu muhimu katika kitabu cha Warumi ili kuelezea dondoo hizi. Tunapendekeza ukariri aya hizi rahisi ili uwe tayari kuwashirikisha wengine habari za Injili kila wakati.

Vielelezo

Kozi Mafunzo ya Msingi > Juma la 7





Gurudumu la Mwanafunzi Larejelewa


Kielelezo hiki kinaonesha jinsi ambavyo kila spoku katika Gurudumu la Mwanafunzi inaunda aina mahususi ya huduma kadiri tunavyokua katika eneo hilo la uanafunzi.
       


Anza kwa kuchora Gurudumu la Mwanafunzi kama kawaida, na upitie upya sehemu mbalimbali. Kisha, angalia jinsi mapendekezo elekezi yote (na vielelezo) ambayo tumejifunza hadi sasa yanavyoingia mahali pake: Kukariri Maandiko (KM), ndiyo msingi wa kumdumisha Kristo katikati ya maisha. Spoku nne zinazounganisha habu kwenye rimu zinajumuisha Kesha la Asubuhi (KA), Shajara ya Maombi (SM), Kutunza Wakati (KW), na Uinjilisti Binafsi (UB). Kwa kifupi, kielelezo hiki kimoja hukusanya pamoja takriban mada zote ambazo umejifunza katika Mafunzo Msingi ya FAST.

Baada ya hapo, chora alama ya mshale inayorefusha kila spoku kuvuka rimu ya nje, na kisha bainisha mishale hii kwa huduma zifuatazo: Maombi hujenga huduma ya maombezi. Kujifunza Biblia hututayarisha kwa ajili ya huduma ya ufundishaji. Utii binafsi hutuongoza kwenye huduma ya kuwausia wengine. Na kuwashirikisha wengine imani yetu kutajenga huduma ya uinjilisti. Kila mwanafunzi anapaswa kujitahidi afikie ubora katika kila moja ya maeneo haya muhimu.