Uinjilisti Binafsi
Kozi Mafunzo ya Msingi > Juma la 6 > Dokezo
 |
|
Dokezo:
Karibu tena kwenye somo lingine la kusisimua. Tumekamilisha baadhi ya mambo muhimu kufikia sasa, lakini tunaendelea na mada nyingine muhimu. Hususan, kijitabu hiki kitaangalia jinsi unavyoweza kuwa shahidi wa Kristo katika ulimwengu wako binafsi. Jifunze mapendekezo yaliyo mbele yako kwa makini, na Mungu anaweza kukupa fursa kadhaa zenye kusisimua kwa ajili ya kuwashirikisha wengine imani yako.
Kulingana na Paulo, “ushirika” wa imani yetu unakuwa “fanisi kwa kutambua kila kitu chema kilicho ndani yetu, katika Kristo” (Filemoni 1:6). Kwa maneno mengine, hakuna kitu chenye nguvu sana kama vile kueleza kwa namna rahisi tu kile ambacho Yesu amefanya maishani mwetu. Hii, hakika, ndiyo maana hasa ya kuwa shahidi: kuripoti kile ambacho tumeona na kusikia. Neno la ushuhuda linaweza pia kuwatia moyo waamini wenzetu. Kwa hivyo washirikishe: na mara nyingi kadiri uwezavyo!
Na kumbuka, ili kupata ufanisi kama shahidi, ni muhimu sana kudumisha maisha yako ndani ya Kristo kupitia kujifunza Biblia, maombi, na utii kwa Neno Lake. Kila kitu ambacho tumejifunza hadi sasa.
Mhariri,
Amefichwa katika Kristo |
These resources are licensed for personal study by . Please do not distribute.
Copyright © 2026, FAST Missions, All rights reserved. WWW.FAST.ST
Uinjilisti Binafsi
Kozi Mafunzo ya Msingi > Juma la 6 > Malengo
 |
Kamilisha Uchunguzi wa Biblia wenye kichwa kisemacho Uinjilisti Binafsi. Kuweza kuwashirikisha wengine Neno la Mungu mara tu unapokutana nao ni sababu nyingine muhimu ya kukariri Maandiko. Kama asemavyo Petro: “Iweni tayari wakati wote..." (I Petro 3:15). |
 |
Aya ya juma hili ni lenye changamoto, likipendekeza angalau maswali kadhaa ambayo sote tunapaswa kujiuliza wakati mwingine: Warumi 1:16. Ikiwa unahisi kuwa na shauku kubwa, jaribu kuongeza aya moja au mbili katika kielelezo cha juma hili. Hata jambo bora zaidi, weka lengo la kujifunza zote tatu ifikapo mwisho wa kozi! |
 |
Soma Mapendekezo ya Kutendea Kazi yanayohusu kusimulia ushuhuda wako binafsi. Tumia muda fulani kutafakari kisa chako mwenyewe cha uongofu kisha jaribu kukiandika. Jiwekee kikomo kwa kile unachoweza kueleza kwa dakika tatu—na si zaidi! Jaribu hilo, kwa kutumia saa. Pia anza kumwomba Mungu akujalie nafasi zaidi ili kuwashirikisha wengine kile ambacho Yesu amefanya maishani mwako. |
 |
Kielelezo cha juma hili kinaitwa Dondoo za Biblia. Kila Mkristo anapaswa kujua jinsi ya kuwashirikisha wengine habari za Injili papohapo. Na punde, nawe utaweza kufanya hivyo! Kwa kweli, endelea kufanyia kazi vielelezo vyako vingine vyote ulivyojifunza hadi sasa. Je, unaweza kubainisha kila moja kikamilifu? |
Si kile afanyacho mtu, bali sababu ya kufanya hivyo
ndiyo huifanya kazi yake iwe takatifu
Uinjilisti Binafsi
Kozi Mafunzo ya Msingi > Juma la 6 > Uchunguzi wa Biblia
Hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwanawe Yesu Kristo. I Yohana 1:3
1. |
"Utume" wa Yesu ulikuwa upi?
Mathayo 18:11
Luka 19:10
I Timotheo 1:15
|
2. |
Yesu aliwafikirije waliopotea? Mathayo 9:36
Je, msukumo wa Yesu kuwafikia waliopotea ulikuwa na nguvu kiasi gani? Yohana 4:34-35
Hivi mtazamo wako kwa waliopotea ungepaswa kubadilikaje ili ufanane sana na Kristo katika eneo hili?
|
3. |
Je, aya hizi hapa chini zinasema wale wanaomfuata Yesu watafanya nini?
Yohana 15:27
Matendo 22:15
|
4. |
Shughuli hii itakuwa pana kiasi gani?
Mathayo 24:14
Matendo 1:8
|
5. |
Shahidi anaagizwa azungumzie nini? I Yohana 1:1-2
Ushuhuda binafsi unaweza kuwa na nguvu kiasi gani? Luka 8:38-40
|
6. |
Tathimini uzoefu wako wa kidini. Je, unaweza kusema wewe binafsi umekutana na Kristo? Eleza.
|
7. |
Je, aya zifuatazo zinapendekeza nini ambacho ni maandalizi muhimu ya kuwashirikisha wengine kisa chako?
II Timotheo 3:15
I Petro 1:23
Zaburi 119:42
Isaya 55:11
|
8. |
Je, uko radhi kiasi gani kujitoa sasa hivi ili kutafuta fursa za kuwashirikisha marafiki na familia uzoefu wako wa kipekee ulioupata katika Kristo? Kwa nini usiandike jibu lako liwe sala fupi kwa Mungu? |
Uinjilisti Binafsi
Kozi Mafunzo ya Msingi > Juma la 6 > Mapendekezo ya Kutendea Kazi
Mpango wa Mungu ni kumfanya kila Mkristo awe shahidi wa uwezo Wake maishani mwake. Naye anatamani kutupatia fursa za kuwashirikisha wengine uzoefu wetu. Lakini Wakristo wengi hawana hata nyenzo za msingi kabisa za kushuhudia—ushuhuda wao binafsi na uwasilishaji wa Injili! Na ni wachache ndio wanaishi maisha yanayolenga kuwafikia wengine. Tunaomba kwamba mapendekezo hapa chini yakupe maarifa sahili kuhusu jinsi unavyoweza kuwaambia marafiki na familia habari za Kristo kwa ufanisi zaidi.
Ulimwengu Wako Binafsi
Kila mmoja wetu ana mduara wa watu tunaokutana nao mara kwa mara. Unaweza kuifikiria hiyo kama ulimwengu wako binafsi. Ni mpango wa Mungu kukutumia ili kuufikia mduara huu. Kwa kweli, unaweza kuwa sehemu pekee ya mawasiliano ya Kikristo kwa baadhi ya watu hawa! Ili kumfanya Kristo awe kitovu cha maisha yako kihalisi, lazima umfanye awe kitovu cha ulimwengu huu binafsi.
Fikiria kuhusu ulimwengu wako binafsi kwa muda: nani aliye karibu nawe unayeweza kumfikia kwa ajili ya Kristo? Jaribu kuandaa orodha ya watu angalau watano ambao si Wakristo. Iwapo huna idadi hiyo ya marafiki wasio Wakristo, huenda ukahitaji kuanza kufikiria njia za kuanzisha mawasiliano zaidi. Je, wapo marafiki wowote wa zamani unaoweza kuwapigia simu au kuwatembelea? Watu walioko kazini au shuleni unaoweza kuanza kuwafahamu? Je, kuna hobi au shughuli fulani unayoweza kufanya ili kuanza kukutana na watu? Endelea kuifanyia kazi hadi uwe na watu angalau wachache kwenye orodha yako.
Kisha, ingiza karatasi ya mahitaji ya maombi kwenye shajara yako ya maombi kwa ajili ya kila mtu na anza kuwaombea kila siku—kwa jina—kwamba Mungu aamshe njaa mioyoni mwao kwa ajili Yake. Mwombe Mungu mahususi akupe fursa za kuwashirikisha wengine ushuhuda wa nguvu za Mungu maishani mwako, na kisha ombea kupata utambuzi wa fursa hizo, na ujasiri wa kuzitumia. Usikubali kutekwa na ile hofu isiyo na mantiki ambayo mara nyingi adui huitumia kunyamazisha. Ukidumisha mwenendo wa urafiki na uchangamfu, Mungu atakufungulia milango ya kuwasimulia kile ambacho Kristo amefanya maishani mwako. Na ikiwa wewe ni mwenye busara na makini, watu hawawezi kuitikia kwa namna hasi. Licha ya hayo, kazi yetu ni kuwa mashahidi wa kile ambacho tumepitia sisi wenyewe. Tafuta fursa hizo za kuwashirikisha wengine!
Ushuhuda Wako Binafsi
Ikiwa unaomba kwa uaminifu na kutafuta kwa bidii fursa za kuwashirikisha wengine neno la ushuhuda, nafasi hizo zitakuja. Jambo la msingi ni kujiandaa. Hii ina maana kutumia muda wa kuufikiria ushuhuda wako, na kuuandika kabisa—mapema.
Bwana alikuongozaje kuwa Mkristo? Au kama ulikulia katika familia ya Kikristo, ni uzoefu gani ulisaidia zaidi kukuimarisha katika uamuzi wako wa kumfuata Kristo? Ushuhuda fanisi unapaswa kuwa mfupi, usiozidi dakika mbili au tatu, na rahisi—usio na istilahi za kidini. Inapaswa pia kubainisha mpango wa wokovu ueleweke dhahiri. Linganisha maisha yako kabla hujawa Mkristo, na maisha yako baada ya hapo, lakini zingatia jinsi hasa ulivyokuwa Mkristo. Fafanua wazi kiasi kwamba asiyeamini anaweza kutambua jinsi ya kuwa Mkristo kwa kusikiliza tu kisa chako. Ikiwezekana, fanyia kazi aya sahihi ya Maandiko—na uikariri.
Mara baada ya kuuandika ushuhuda wako binafsi, fanya zoezi la kumweleza rafiki Mkristo. Baadaye, unaweza kuandaa shuhuda za ziada za jinsi ambavyo Mungu amekusaidia katika maeneo maalumu kama vile upweke, woga, au kukosa kusudi maishani. Hakuna kitu chenye nguvu zaidi, au kisichoweza kupingika, kuliko ushuhuda halisi wa mtu binafsi!
Kidokezo cha Kukariri Maandiko: Je, Mungu amekuwa akifanya kazi maishani mwako kupitia aya ambazo umekuwa ukikariri? Kuwasimulia waumini wenzako ushuhuda kuhusu kile ambacho Mungu anakufundisha kunaweza pia kuwa na nguvu—na kutia moyo. Na ikiwa humhimiza mtu fulani kuanza kukariri pia, inaweza kuwa badiliko kubwa maishani mwake! Kwa hiyo waeleze wengine jambo unalojifunza katika Neno la Mungu katika kila fursa kadiri uwezavyo.
Umuhimu wa Kujitoa
Epuka kuanguka katika mtego wa kufikiria kushuhudia kutatokea tu kiasili iwapo unatumia muda pamoja na Kristo. Lazima tutumie muda pamoja na Kristo, ndiyo—lakini lazima pia tukusudie kwa dhati na tuwe makini katika juhudi zetu za kuwashirikisha wengine habari za Kristo. Itahitaji
azma, kujinasibisha na Bwana daima katika kila fursa, na inaweza kuwepo gharama wakati fulani. Lakini maagizo yetu yako wazi. Je,
hutaazimu kuwa shahidi hai wa Kristo?
Uinjilisti Binafsi
Kozi Mafunzo ya Msingi > Juma la 6 > Kielelezo
Dondoo Muhimu za Biblia